WAKAZI wa wilaya za Tarime na Rorya
mkoani Mara, wameshauri kupunguzwa kwa posho za wajumbe wa Bunge maalumu
la Katiba kutoka Sh 300,000 hadi Sh 170,000 ambazo walisema ni za
kawaida kwa vikao vya Bunge.
Wamewaomba pia wajumbe hao ambao
wamekwenda kuwawakilisha wenzao kuweka maslahi ya Taifa mbele na kuacha
tamaa za kujipatia fedha nyingi ambazo ni kodi za wananchi.
Waliotoa ushauri huo ni Sigirya Mwita
ambaye ni Mwenyekiti wa CCM wa Kata ya Pemba, Peter Mwera ambaye ni
Diwani wa CCM wa Kata ya Mriba na Nyangoko Paulo ambaye ni Mwenyekiti wa
Kijiji Sirari kupitia Chama cha Chadema.
Wengine ni wananchi wa kawaida Otieno
Igogo, Matiko Majani, Elizabeth Mseti, Ores Lameck, Kansela Sereria,
Maria Bhoke na Gimase Marwa.
Viongozi na wananchi hao walisema
hawakubaliani na maombi ya wabunge hao ya kuomba serikali kuwaongezea
posho na badala yake wapunguziwe kutoka Sh 300,000 za sasa hadi Sh 170,
000 ambazo ndizo zinazokubalika kisheria kwa vikao.
“Katiba hii wanayoijadili ni ya
Watanzania wote hata wao wamo na familia zao. Hawakupendekezwa kwenda
kujitafutia mitaji na kutaka kuhujumu uchumi wa nchi. Kuna baadhi yao
humo hawapati au kuzalisha hata Sh 100,000 kwa siku kwao.
“Kisingizio kuwa ni wajumbe wa Bunge
maalumu la Katiba hakina mashiko.Tunaomba Serikali kutowaongeza posho
hizo badala yake zipunguzwe kwani fedha hizo ni za wananchi ambazo
zingine hupelekwa katika kutekeleza miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi
wa madarasa, nyumba za walimu, barabara, kuchimba visima vya maji na
kuwasomesha wanafunzi waliokwama kuendelea na masomo,” walisema kwa
nyakati tofauti.
No comments:
Post a Comment