BARAZA la Taifa la Mitihani (Necta) limetoa ufafanuzi kuhusu viwango
vya ufaulu, alama ya chini ya ufaulu na ufaulu wa jumla, ambavyo
vimetumika kwa mara ya kwanza mwaka huu.
Akifafanua kuhusu viwango vya ufaulu jana, Kaimu Katibu Mtendaji wa
Baraza hilo, Dk Charles Msonde alisema kuanzia mtihani wa kidato cha nne
ya mwaka 2013, Baraza limetumia utaratibu wa makundi saba, tofauti na
miaka ya nyuma, ambapo walikuwa wakitumia makundi matano.
Alitaja makundi hayo na alama zake kwenye mabano kuwa ni A (75-100)
yenye pointi 1; B+ (60-74) yenye pointi 2; B (50-59) yenye pointi 3;
C(40-49) yenye pointi 4; D (30-39) yenye pointi 5; E (20-29) pointi 6 na
kundi F (0-19) yenye pointi 7.
“ Utaratibu huu umelenga kupunguza mlundikano mkubwa wa alama katika
kundi mmoja.” “Idadi ya makundi ya ufaulu hutofautina kati ya nchi na
nchi kulingana na mahitaji, mfano Kenya wanamakundi 12, Uganda, Malawi
na nchi za Afrika Magharibi wanamakundi tisa,” alisema.
Alisema kutokana na makundi hayo, kiwango cha mwisho cha ufaulu ni
gredi D na kiwango cha juu ni A kwa somo husika na watahiniwa waliopata
gredi E na F wanakuwa hawajafaulu somo husika.
Akizungumzia upangaji wa madaraja ya ufaulu, Msonde alisema
yamepangwa kwa mujibu wa Kanuni za Mitihani Kifungu cha 20 (1-6),
ambacho kinaeleza kuwa ufaulu katika daraja la Kwanza hadi Tatu
unapangwa kwa kuzingatia jumla ya pointi.
Alisema kwa upande wa daraja la Nne, kanuni inataka kupangwa kwa
kuzingatia ufaulu wa chini ambao ni gredi D katika masomo yasiyopungua
mawili au ufaulu kwa kiwango cha chini ya gradi C katika somo moja.
Hata hivyo, kanuni inaelekeza kuwa ufaulu wa grade A hadi C utakuwa
ni ufaulu wa ‘Credit’ na gredi D inaesabika kuwa ni ‘pass’ na gredi E na
F ni alama za kufeli.
“Tumepokea maswali mengi sana hasa kwa katika daraja la Nne maana
wengine wanaonekana kuwa na pointi za daraja sifuri lakini wanaonekana
kuwa katika daraja la Nne, kwa kanuni daraja la Nne hupangwa kwa alama
za chini na si kwa pointi,” alisema.
Msonde alitolea mfano mtahiniwa ambaye amefanya masomo saba na
amepata alama D katika masomo mawili na masomo matano amepata F, kwa
pointi mtahiniwa huyo ataonekana kuwa na pointi 45 ambazo ni za daraja
Sifuri, lakini kutokana na kuwa na D mbili kanuni inamtaka kupewa daraja
la Nnne.
Aidha, Msonde alisema kuwa ufafanuzi wa sifa za kujiunga na mafunzo
katika ngazi mbalimbali kwa kutumia mfumo huu utatolwa na Kamishna wa
Elimu.
No comments:
Post a Comment