Sehemu ya Barabara ya Mlandizi-
Chalinze, ikiwa imeharibika kutokana magari makubwa kuzidisha uzito na
kusababisha uharibifu huo.Picha na Maktaba
- Hasara hiyo inatokana na uharibifu wa barabara za lami ambao unachangiwa kwa kiasi kikubwa na malori yanayozidisha uzito wa mizigo kinyume cha sheria na kanuni namba 7 (3) ya Sheria ya Usalama Barabarani ya 2001.
Dar es Salaam: Uamuzi wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuruhusu malori makubwa
ya mizigo yaendelee kuzidisha uzito wa mizigo, umetajwa kuwa ni hatari na
utaisababishia Serikali hasara ya mamilioni ya fedha.
Hasara hiyo inatokana na uharibifu
wa barabara za lami ambao unachangiwa kwa kiasi kikubwa na malori yanayozidisha
uzito wa mizigo kinyume cha sheria na kanuni namba 7 (3) ya Sheria ya Usalama
Barabarani ya 2001.
Ujenzi wa barabara ni wa gharama
kubwa na hata ukarabati wake umekuwa ukitengewa mabilioni ya fedha za
walipakodi kutokana na uharibifu unaofanywa.
Mathalani katika bajeti yake ya
2013/14, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, imetenga kiasi cha Sh314.535
bilioni kwa ajili ya mpango wa matengenezo ya barabara kuu na barabara za
mikoa.
Kiasi hicho cha fedha ambacho ni
zaidi ya robo ya bajeti nzima ya wizara hiyo kwa mwaka, kinatosheleza kujenga
barabara mpya ya lami yenye urefu wa kilometa zipatazo 315, kwa makadirio ya
kilometa moja kugharimu Sh1 bilioni. Katika mwaka huu wa fedha, bajeti nzima ya
Wizara ya Ujenzi ni Sh1.226 trilioni.
Kauli ya Dk Magufuli
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli,
aliwahi kunukuliwa akisema ataendelea kusimamia sheria ya barabara namba 30 ya
mwaka 1973, hadi anaingia kaburini kwa kuhakikisha hakuna magari ambayo
yanazidisha uzito na kuharibu barabara.
“Nchini Ujerumani, uzito wa magari
yote ni tani 40, Uingereza tani 40, Ufaransa 40, Urusi 38 lakini Tanzania tani
56, wakati mwingine tunakamata hadi tani 96,” alisema Dk Magufuli.
Hata hivyo, ujasiri wa Dk Magufuli
ulizimwa na amri ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliyetengua agizo la waziri huyo
na kuamua kuruhusu magari yenye uzito uliopitiliza kuendelea kutumia barabara.
Wasemaji wa Serikali
Ofisa Habari wa Wizara ya Ujenzi,
Martin Ntemo alisema suala hilo wameliachia Ofisi ya Waziri Mkuu. “Hilo suala
liko Ofisi ya Waziri Mkuu, siwezi tena kulizungumzia,” alisema Ntemo kwa kifupi.
Hata hivyo, Katibu Mkuu, Ofisi ya
Waziri Mkuu, Dk Florence Turuka alisema siyo sahihi kusema kwamba Waziri Mkuu
amevunja sheria kwani ilikuwa ni lazima serikali ichukue hatua jumuishi kwa
kuwashirikisha wadau husika.
Habari kutoka Mwananchi
No comments:
Post a Comment