IDADI ya mifugo inayokufa kwa kula
mifuko ya nailoni inazidi kuongezeka katika Kata ya Hombolo. Diwani wa
Kata ya Hombolo Manispaa ya Dodoma, Mussa Kawea katika mahojiano na
mwandishi wa habari hizi alisema katika kipindi cha wiki mbili mifugo
inayokufa imefikia 500 huku wafugaji wengine wakiingia katika umasikini
kwa kupoteza ng'ombe zaidi ya 20.
Taarifa za mwanzo zilisema kwamba idadi ya mifugo iliyokufa kwa kula mifuko hiyo ilikuwa 65.
Alisema mifuko hiyo ambayo imezagaa sana
eneo la Hombolo kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu
zilizochangiwa na uwepo wa Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo imekuwa
chanzo kikubwa cha kuwatia katika umasikini.
Kawea alisema licha ya mvua kuanza
kunyesha na majani kuongezeka lakini ng’ombe wamekuwa wakila mifuko hiyo
inayozagaa ovyo kutokana na kuwa na ladha ya chumvi chumvi.
Alisema pamoja na wafugaji kulifikisha
suala hilo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani lakini hakuna kitu
chochote kilichofanyika mpaka sasa.
Alisema ni muhimu kwa Serikali ikapiga
marufuku utengenezaji wa mifuko hiyo kutokana na kuwa na madhara makubwa
kwa mifugo huku akiwataka wananchi wenye mazoea kuhakikisha kwamba
hawaitupi hovyo na wanaichoma.
“Hali hii inatishia umasikini kwa
wafugaji tunaomba Serikali kuangalia suala hili kwa makini. Alisema,
kutokana na vifo vya ng’ombe vinavyotokea kila mara wafugaji wa maeneo
hayo wameitaka Serikali kutimiza maagizo wanayoyatoa ikiwemo lile la
kupiga marufuku matumizi ya mifuko hiyo.
“Serikali ilipiga marufuku utengenezaji
wa mifuko ya rambo na kuagiza viwanda vitengeneze mifuko ya karatasi
ambayo ni rahisi kuharibiwa baada ya matumizi lakini agizo hilo
linaonekana halijazingatiwa,” alisema.
Alipohojiwa hivi karibuni juu ya athari
anazopata ng’ombe anapokula mfuko wa plastiki Daktari wa Mifugo mkoani
hapa, Goodluck Ndaweka alisema ng’ombe anapokula mfuko wa plastiki
husababisha mfuko ule kwenda kufunga utumbo mwembamba jambo ambalo
husababisha chakula anachokula kishindwe kupita.
Alisema kutokana na hali hiyo ng’ombe hukonda na hali hiyo hupelekea kifo chake.
No comments:
Post a Comment