“Tulionywa na Amerika kabla
ya uchaguzi kwamba tukiwachagua Uhuru na Ruto tungejuta na sasa
tumejuta. Wakenya milioni sita walimchagua Uhuru. Kweli sikio la kufa
halisikii dawa.
Dalili ya mvua ni mawingu. Mawingu yanayofunika anga la Kenya wakati huu
yanaashiria kwamba mvua itakayonyesha itasababisha mafuriko katika
nyanja za kisiasa na kiuchumi.
Ni kwa sababu hii wote wanaojali hatima ya nchi hawana budi kujitokeza
kimasomaso ili kuona athari za vitendo vya Serikali ya Jubilee kwa nchi
na kutafuta jinsi ya kuepukana nazo.
Jukumu hili liko juu ya mabega ya vyama vya upinzani haswa Muungano wa
CORD unaoongozwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga, Kalonzo Musyoka
na wengine.
Ni wakati wa CORD kuonyesha kuwa haiwezi kusita kueleza na kuihakiki
Serikali ya Uhuru Kenyatta pia ni dhabiti na kwamba viongozi wake
watakuwa wanazungumza kwa sauti moja wanapoikosoa Serikali.
Wengi walitarajia kwamba viongozi wa Cord wangetengana baada ya uchaguzi
mkuu, lakini Raila, Kalonzo Musyoka na Moses Wetangula bado ni
wanachama wa CORD.
Historia ya vyama vya kisiasa nchini inaonyesha kwamba, viongozi huunda
vyama kwa lengo la kushinda uchaguzi lakini baada ya miezi michache
vyama hivyo husambaratika.
Kwa mfano, kiongozi wa United Democratic From (UDF), Musalia Mudavadi
anajitayarisha kujiunga na Serikali ya Uhuru kama waziri. Gazeti moja la
kila siku limenukuliwa likiripoti kwamba, Mudavadi hivi karibuni
ataingizwa kwenye serikali.
Tatizo nini?
Upinzani umegundua kwamba Serikali ya Jubilee imeanza kuonyesha kucha
zake miezi michache baada ya kujifanya kwamba inafuata sheria na kulinda
Katiba. Ilifanya hivyo kwa kuteua Baraza la Mawaziri inavyotakiwa
kisheria, lakini sasa mambo yamebadilika.
Uhuru na Makamu wake,William Ruto, wameonyesha kuwa hawajali lolote zuri
linaloiweka Kenya kwenye jukwaa la mataifa yanayowalinda wananchi wake.
Kwa wiki moja iliyopita, Upande wa Serikali bungeni umepitisha miswada
miwili inayorudisha nyuma hatua nzuri zilizokuwa zimepigwa.
Kumekuwa na kilio kikuu kutoka kwa Wakenya kuhusu hatua ya Serikali
kutaka kuzima uhuru wa wanahabari na pia kukata msaada kwa mashirika
yasiyo ya kiserikali kutoka kwa mashirika ya maendeleo ya nchi za Ulaya
na Magharibi.
Si jukumu la upinzani kuisifu Serikali na kuchochea maendeleo. Huu si
wakati wa kupakana mafuta kwenye mgongo wa chupa kwani mshuka ngazi na
mpanda ngazi kamwe hawawezi kushikana mikono.
Jukumu lake ni kuhakikisha Serikali inafuata mkondo unaofaa
inapoendesha shughuli zake. Ni jukumu la kusukuma Serikali ili izingatie
ahadi zake zote ilizotoa kwa Wakenya wakati wa kampeni na uchaguzi na
hatimaye wakati wa kuapishwa kwake Uhuru na Ruto Aprili 9, 2013.
Kuna orodha ndefu ya mambo yasiyofurahisha wengi nchini, na chimbuko la
haya yote ni Serikali ya Jubilee. Wakenya bado wanajiuliza maswali
kuhusu jinsi mkuu wa majeshi alivyokuwa amekana kwamba kikosi chake
hakikupora mali wakati wa mashambulizi ya Westgate.
Maji yalipozidi unga, Serikali ilikiri kwamba kweli, wanajeshi walikuwa
wamepora. Kwanini Wakenya wachukuliwe kana kwamba ni majuha? Mbona
Serikali haikukiri mara moja kwamba makosa yalifanyika badala ya
kujaribu kuficha ukweli?
Muswada wa ushuru wa chakula na bidhaa nyingine muhimu ulipelekea
kupanda kwa gharama ilhali mapato ya wananchi ni yale yale. Baada ya
kilio kutoka kwa raia, Serikali ilitoa sababu kwamba haikuwa inalenga
bidhaa muhimu kama vile maziwa na mikate walipoupitisha muswada huu.
Sote twafahamu ni kina nani wanaoshikilia sekta ya maziwa na wangefaidi
kutokana na kuongezeka kwa bei ya maziwa na bidhaa nyingine.
Isitoshe, kuna maswali mengi kuhusu jinsi pesa za umma zinavyotumiwa.
Tangu vikao vya kesi zinazomkabili Ruto ianze The Hague zaidi ya mwezi
mmoja uliopita, wabunge na wafanyakazi wa umma wamekuwa wakimtembelea
kiongozi huyu kila wiki ili kumpa moyo kortini.
Je, wabunge na wafanya kazi wa umma wanaosafiri kila mara kumtembelea
Makamu wa Rais wanafanya hivyo kwa kujigharamia au fedha za umma ndizo
zinatumiwa?
Pia, Waziri wa Masuala ya Nchi za Nje, Amina Mohammed amekuwa kiguu na
njia tangu ateuliwe. Kazi ya kutumikia wananchi imewekwa kando badala
yake kesi ya Uhuru imepewa kipaumbele.
Mohammed ametembelea nchi nyingi kutafuta uungwaji mkono kwa kesi hizi.
Uhuru na Ruto walikuwa wamewahakikishia wananchi wakati wa kampeni na
hata walipokuwa wakifanya kampeni kwamba, kesi zao ni za kibinafsi.
Lakini sasa zimekuwa za kitaifa na hata kimataifa. Wakenya wangetaka
kujua pesa hizo zote za nauli na kadhalika zinalipiwa na nani.
Shirika moja lisilo la kiserikali, Mars Group linaunga mkono juhudi za
Upinzani za kutaka kujua jinsi safari hizi za kila mara
zinavyogharamiwa. Mkurugenzi Mkuu wa Mars Group Kenya, Mwalimu Mati
anataka Uhuru aeleze ikiwa matumizi ya pesa kwenye shughuli za kibinafsi
kama hizi zilijadiliwa kama muswada katika Bunge la kitaifa na
kupitishwa.
Upinzani ungetaka kujua mfuko wa fedha unaotumiwa na Uhuru na Ruto
kuzuru nchi mbalimbali za Afrika kukutana na viongozi wa kisiasa barani
ili wawaunge mkono kuhusiana na kesi za Hague.
No comments:
Post a Comment