Wajumbe
wa Bunge Maalumu la Katiba wakiingia bungeni mjini Dodoma jana
kuhudhuria semina ya kuchangia taarifa ya Kamati ya Kumshauri Mwenyekiti
wa Muda wa Bunge kuhusu Kanuni. Picha na Silvan Kiwale
Hofu
imetanda kuhusu uwezekano wa kuvunjika kwa Bunge Maalumu la Katiba,
kutokana na hatua ya CCM kutumia wingi wao kutaka kupitisha utaratibu wa
kupiga kura za wazi.
Baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo, wameshauri njia pekee ya kunusuru mchakato huo ni kwa CCM kukubali kukaa meza ya mazungumzo.
Wakati
wajumbe hao wakitoa angalizo hilo, taarifa zilizopatikana jana mjini
Dodoma zilisema CCM, wameitisha kikao cha dharura cha wajumbe wake wote
leo saa 8:00 mchana kwa agenda ambayo bado ni siri.
Habari
hizo zinadai kuwa wajumbe ambao ni Wabunge na Wawakilishi wa Baraza la
Wawakilishi Zanzibar, wametumiwa ujumbe mfupi wa simu (SMS) wakitakiwa
kuhudhuria kikao hicho bila kukosa.
“Mambo
muhimu yatajadiliwa, Mwenyekiti wa Cocas (umoja wa wabunge) anasisitiza
mhudhurie bila kukosa, mahudhurio yatazingatiwa,” unasomeka ujumbe huo
ambao gazeti hili limeuona.
Baadhi
ya wabunge wa CCM hususan wanaotoka Kanda ya Ziwa wanaounga mkono kura
ya siri, walidai kuwa kikao hicho huenda kina nia ya kuwatisha ili
walegeze msimamo wao.
“CCM
wanaogopa kura za siri kwa sababu moja tu, wakiiruhusu watakuwa hawana
control (udhibiti) wa wajumbe kutoka Zanzibar ambao wengi wanataka
Serikali tatu,” alidokeza mbunge mmoja ambaye hata hivyo, hakutaka jina
lake litajwe.
Mbunge
huyo alisema kwa tathmini yake, kama utaratibu wa kura za siri utapita,
karibu asilimia 80 ya wajumbe wote kutoka Zanzibar, watapiga kura ya
kupitisha rasimu ya muundo wa Serikali tatu.
“Kwa
hiyo CCM haitaki kabisa utaratibu wa kura za siri, wanataka kura za
wazi ama kura ya dhahiri ili waweze kuwa na udhibiti wa wajumbe ili
tusitoke nje ya msimamo wao,” alidai mbunge huyo.
Hata
hivyo, wakati CCM ikishikilia msimamo wa kura za wazi katika kupitisha
rasimu hiyo, wabunge wake wengi wa Tanzania Bara na wale wa Zanzibar
wanataka upigaji wa kura za siri.
Akizungumza
na gazeti hili jana, James Mbatia alitahadharisha kuwa msimamo wa CCM
kulazimisha kura za wazi, siyo kuwatendea haki Watanzania na huenda
ikawa chanzo cha machafuko na kukwama kupatikana Katiba Mpya.
“Kulazimisha
matakwa ya CCM badala ya wananchi itakuwa ni chanzo cha machafuko na
Watanzania hatuko tayari kwa machafuko wala kuona damu ya Mtanzania
inamwagika,” alisema Mbatia
Mbatia
aliongeza kusema; ni vizuri hiyo Rasimu ya Katiba tuiboreshe, tupunguze
mengine na CCM kama wana hoja wazilete bungeni na ziwe hoja zenye
mashiko siyo vitisho, hatutavuka hapa.”
Mbatia
aliwataka baadhi ya viongozi wa CCM kutokujifanya wanamfahamu sana Baba
wa Taifa, Mwalimu Nyerere kuliko anavyomfahamu Joseph Butiku na Joseph
Warioba walioshiriki kukusanya maoni ya Watanzania kwa ajili ya Katiba
Mpya.
“Nyerere
hakuwa na mawazo mgando, alikuwa na fikra pevu zilizokuwa zinakwenda na
wakati na ndiyo maana alikubali mapendekezo ya Watanzania asilimia 20
waliotaka mfumo wa vyama vingi,” alisema.
Alisema
kama kweli viongozi wa CCM wana dhamira ya kweli na muundo wa Muungano,
basi wafute kwanza mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ili sasa
wazungumze.
“Mabadiliko
ya 10 ya Zanzibar yalitamka kuwa Zanzibar ni nchi na ina mipaka yake na
mwenye mamlaka ya kuigawa Zanzibar ni Rais wa Zanzibar… hilo tu tayari
walikuwa wamevunja Katiba ya Muungano.
Mbatia
alisema ibara ya 2(A), ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, imeweka bayana
kuwa pale Rais anapotaka kuigawa Zanzibar, atashirikiana na Rais wa
Tanzania Zanzibar.
“Kwa
katiba hiyo, Rais wa Zanzibar amepora ardhi ya JK (Rais Jakaya Kikwete)
kwa hiyo walishavunja Muungano kisheria… kwa maneno mengine mabadiliko
hayo ni uhaini dhidi ya Katiba ya Muungano.”
Mbatia
alisema katiba siku zote ni tendo la maridhiano na kuitaka CCM kuingia
katika maridhiano, kama kweli ina nia thabiti ya kuwapatia Watanzania
katiba badala ya kutumia wingi wao kuififisha.
Mwenyekiti
huyo alisema anawashangaa CCM kwamba wao ndiyo walioanzisha mchakato wa
katiba na kuunda tume, mchakato ukaendeshwa na Serikali ya CCM halafu
wanayakataa mapendekezo yake.
Mbatia
alisema tume tano zilizoundwa kwa ajili ya suala moja tu la muundo wa
Muungano, zilikuja na mapendekezo ya Serikali tatu na kushangaa CCM sasa
kuhoji uadilifu wa Tume ya Jaji Warioba.
Tangu
kuanza kwa Bunge Maalumu la Katiba, bunge hilo limetumia takriban siku
16 sasa katika kutunga rasimu za kanuni na kubwa linalobishaniwa ni
utaratibu wa upigaji wa kura.
Mapendekezo
ya awali ya Kanuni za Uendeshaji wa bunge hilo, zilipendekeza upigaji
kura uwe wa siri na hata wajumbe walipochangia na CCM kung’ang’ania kura
za wazi, bado kamati ilikuja na pendekezo la kura za siri.
Hata
hivyo wajumbe wengi wanaotoka CCM walipinga kwa nguvu zote kura za siri
wakitaka za wazi na suala hilo kurudishwa kwenye kamati, lakini hadi
juzi kamati ilishindwa kuafikiana.
Kutokana
na suala la upigaji kura kuonekana ni tata, kamati iliyoundwa kupitia
kauni hizo, juzi iliamua kurudisha suala hilo kwa Bunge la Katiba ili
ilifanyie uamuzi.
Oluoch ataka hati ya Muungano ipelekwe mezani
Mjumbe
wa Bunge Maalumu la Katiba, Ezekiah Oluoch, ameuchambua Mchakato wa
Mabadiliko ya Katiba na kutaja kitendo cha wajumbe wa Bunge hilo
kutokugawiwa hati ya Muungano kuwa moja ya kasoro kubwa zinazoukabili.
Akizungumza
katika mahojiano maalumu na gazeti hili jana, Oluoch alihoji mantiki ya
wajumbe wa Katiba kujadili Muungano, wakati hawana hati ya Muungano
iliyosainiwa na waasisi wake; Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani
Karume.
“Mimi
nililiona hilo mapema, nikaenda kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji
Frederick Werema, nikamuuliza kama atagawa hati ya Muungano kwa wajumbe,
lakini inaonekana hakuna mpango huo. Sasa tunajadilije Muungano wakati
hatujui msingi wake,” alihoji.
Oluoch
alisema nguzo ya Bunge la Katiba ni Muungano na kwamba matunda yake
yataonekana kama kumewekwa mazingira mazuri ya kuujadili.
“Lakini
utajadilije Muungano wakati huna nakala ya article of Union (hati ya
Muungano). Mimi nilidhani ili kwenda vizuri wajumbe wapewe kwanza nakala
ya hati hizo,” alisema.
Wawakilishi Zanzibar washikana mashati
Mwinyi
Sadallah anaripoti kutoka Zanzibar kuwa wakati Bunge la Katiba linaanza
kesho mjini Dodoma, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW)
wamesema kuna waraka bandia umesambazwa ukieleza Baraza hilo limeazimia
kwa pamoja kutaka mamlaka kamili ya mataifa ya Zanzibar na Tanganyika.
Waraka
huo umesababisha mgogoro na kutoelewana kwa wajumbe katika kamati ya
uongozi chini ya Mwenyekiti wake Spika Pandu Ameir Kificho na Katibu wa
kamati hiyo Yahaya Khamis Hamad, baada ya kujitokeza hadharani baadhi ya
wajumbe wakisema waraka huo umeghushiwa na hawautambui.
Akizungumza
na Mwananchi Spika Pandu Ameir Kificho hakukubali au kukataa kuwepo kwa
waraka huo na badala yake akasema atakuwa tayari kuutolea maelezo
atakapofika ofisini kwake, licha baadaye alipopigiwa simu na kupokea
akasema tena kuwa atautolea majibu alasiri, jana jioni.
“Sina
la kusema kwa sasa, acha nifike ofisini nitakueleza kuhusu jambo
hilo...niache ndugu yangu nifike ofisni kwangu kwanza. Tafahali niko
njiani hivi sasa, siko tayari kuuzungumzia waraka huo au mwingine…niache
nitakwambia baadaye ,” alisema Spika Kificho ambaye ni Mwenyekiti wa
muda wa Bunge la Katiba.
Hata
hivyo, alipopigiwa simu Katibu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Yahya
ili atoe maelezo ya kina kuhusu waraka huo iwapo BLW Zanzibar lilitoa
azimio lake na kuliwasilisha kwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabailiko ya
Katiba Jaji Joseph Sinde Warioba kutaka mfumo wa serikali tatu. Awali
alikubali na kukana akisema inawezekana si waraka huo anaouzungumzia ila
BLW limependekeza kupatikana kwa mamaka huru ya Tanganyika na Zanzibar.
“Hapana
waraka wa Azimio la Baraza kutaka mfumo wa serikali tatu
siutambui.Lililofanyika ni kutaka mamlaka huru za Tanganyika na
Zanzibar, pia kuna mambo mengi humo, sitaki unihukumu kwa waraka ambao
sioni katika simu. Ingefaa niuone kwa macho yangu kama ndiyo wenyewe au
la,” alisema Yahya.
Akiuzungumzia
waraka huo, Mnadhimu ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Baraza
hilo, Salmin Awah Salmin (Magomeni), alisema waraka upo ila ni wa
kughushiwa kwa sababu hakuna kikao cha kamati ya uongozi kilichowahi
kukaa na kutoa azimio la pamoja juu ya aina gani ya Muungano unaotakiwa
kuzingatiwa katika uundwaji wa Katiba Mpya ya Tanzania.
Salmin
alisema kuwa waraka huo umeandikwa kwa niaba ya kamati ya uongozi ya
Baraza la Wawakilishi Zanzibar na una saini ya Spika wetu Kificho jambo
ambalo alisema si la kweli bali ni la upotoshaji mkubwa.
Alisema
kumbukumbu zinaonyesha tangu kuanza kwa mjadala wa mabadiliko ya
katiba, BLW Zanzibar halijatoa msimamo wa pamoja na kuzingatiwa, badala
yake kila upande wa kisiasa na kiitikadi umekuwa na maoni yake ikiwa ni
pamoja na kambi ya upinzani kutaka mfumo wa Serikali ya Muungano wa
mkataba na chama tawala kusimamia mfumo wa Serrikali mbili.
Mnadhimu
huyo alisema baaada ya kufuatilia kwa undani aligundua kuwa kuna watu
watano ndiyo waliojifungia na kuutengeneza waraka huo ukitumia jina la
Kamati ya Uongozi na kwa niaba ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar
kuutayarisha na kujenga hoja wanazozitaka wao kwa matakwa yao.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment