RAIS Jakaya Kikwete hajaongeza posho kwa wajumbe wa Bunge Maalum la
Katiba kutoka Sh 300,000 za sasa na kueleza kuwa hajawahi kupokea maombi
ya nyongeza ya posho hiyo.
Badala yake amefanya marekebisho ya mpangilio wa posho hizo ambapo itabaki Sh 300,000 hiyo hiyo ya awali.
Maelezo hayo ya Rais Kikwete yaliyotolewa kupitia kwa Mkurugenzi wa
Mawasiliano wa Ikulu, Salva Rweyemamu yanabainisha kuwa maombi kutoka
katika bunge hilo aliyopokea ni kufanyia marekebisho mpangilio kwa posho
hiyo na amekubali na kuruhusu kufanya kama wajumbe walivyoomba.
“Kilichoombwa si nyongeza ya posho bali ni ile Sh 300,000 kupanga katika mpangilio tofauti na awali,” alisema.
Katika mpangilio wa awali katika posho ya Sh 300,000 ilikuwa posho ya
kujikimu Sh 80,000 na Sh 220,000 posho maalum ya kuhudhuria vikao.
Katika posho hiyo ya kuhudhuria vikao iligawanywa posho ya dereva
kati ya Sh 40,000 na Sh 45,000 kwa siku, usafiri wa ndani yaani mafuta
au teksi, mawasiliano na matumizi mengine binafsi.Mchanganuo mpya
haukutolewa na Ikulu.
Mgawanyo huo uliopitishwa na Rais uliwasilishwa kwake na Kamati ya
Kushughulikia Posho iliyoundwa na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hilo,
Pandu Ameir Kificho.
Kamati hiyo ilikuwa na wajumbe sita nao ni William Lukuvi, Mohamed
Abood Mohamed, Freeman Mbowe, Paul Kimiti, Jenister Mhagama na Asha
Bakari.
Kamati hiyo iliyoanza kazi Februari 19 iliongozwa na mambo manne
likiwamo la uhalisia wa gharama za maisha mjini Dodoma na aina ya
wajumbe walioteuliwa kwa kuainisha pato lao kabla ya kuwa wajumbe wa
Bunge.
Pia sheria kuhusu taratibu za posho, uwazi wa posho zinavyotolewa na
ulinganisho wa malipo ya kuzingatia aina za wajumbe. Kamati baada ya
kujiridhisha iliwasilisha mapendekezo yake kwenye mamlaka hiyo, ili
itafakari mapendekezo hayo na kutoa maelekezo.
Rweyemamu alieleza msimamo huo wa Rais kuhusu posho kutokana na kauli
iliyotolewa juzi na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania
(TUCTA) Mkoa wa Dodoma kusema iwapo wajumbe hao wataongezwa posho na
mamlaka za uteuzi watafanya maandamano ya amani nchi nzima.
Aidha kumekuwapo na taarifa kuwa posho hiyo imeongezwa na kufika Sh 500,000.
“Mamlaka ya uteuzi haiwezi kuongeza posho kutokana na kuwa haijawahi
kupokea maombi ya ongezeko la posho hiyo na wala haijaongeza posho hiyo
kama ilivyoelezwa katika baadhi ya vyombo vya habari,” alisema
Rweyemamu.
Chimbuko la hoja Februari 19 ikiwa ni siku ya pili ya kikao cha Bunge
Maalumu, Richard Ndassa Mbunge wa Sumve, ndiye aliibua suala hilo la
posho akisema Sh 300,000 kwa siku wanayolipwa wajumbe wa Bunge Maalumu
la Katiba ni ndogo.
Pia alidai wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameongezwa posho na SMZ
jambo ambalo linaleta tofauti bungeni lakini baadaye Katibu wa Baraza la
Wawakilishi, Yahya Khamis Hamad, alikiri wawakilishi walidai nyongeza
hiyo ya posho lakini SMZ haikuwajibu.
Wawakilishi hao walidai wanapokuwa nje ya SMZ wanalipwa Sh 200,000
hivyo baada ya kufika kwenye Bunge Maalumu na kubaini posho ya kujikimu
ni Sh 80,000, waliwasilisha maombi waongezwe kiasi kinachopungua,
ambacho ni Sh 120,000 kwa siku.
Akiungwa mkono na Mbunge wa Kishapu, Suleiman Nchambi, walihoji
sababu za wao kupewa posho hiyo wakati wajumbe wa Tume ya Marekebisho ya
Katiba walilipwa Sh 500,000 walipokuwa wakikusanya maoni.
Kwa mujibu wa wanaotaka nyongeza, mchanganuo wa matumizi yao ni
kwamba hadhi ya hoteli wanayopaswa kulala ni ya kuanzia Sh 70,000. Pia
wanahitaji mafuta ya gari, kulipa madereva na kutoa fedha kwa watu
mbalimbali wanaowaomba msaada.
Kutokana na madai hayo ya wajumbe ya nyongeza ya posho kulizuka
malalamiko kutoka kwa watu mbalimbali wanaopinga nyongeza hiyo kwa madai
iliyopo ni kubwa na wengine wanasema inatosha.
Miongoni mwa waliopinga hadharani nyongeza hiyo kutoka ndani ya bunge
hilo ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini Kabwe Zitto, Julius Mtatiro, Mbunge
wa Karatu Israel Natse, Naibu Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba na Mbunge
wa Nkasi Mohamed Kessy.
No comments:
Post a Comment