SAKATA la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe
(Chadema), kutuhumiwa kutumia vibaya madaraka yake, limeweka ndoa za
wabunge shakani.
Mbowe juzi alituhumiwa na Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba
(CCM), kubadilisha ziara ya Mbunge wa Viti Maalum, Joyce Mukya
(Chadema), aliyotumwa na Bunge nje ya nchi huku akiwa amechukua posho,
asiende alikotumwa badala yake aende Dubai katika Falme za Kiarabu na
kurejea nchini.
Wakimtetea Mbowe, baadhi ya wabunge wa Chadema walifikia hatua kusema
huo ni uhusiano binafsi na kuongeza kuwa kama na wao wakianza kutaja,
kila mbunge ana uhusiano wa kifuska bungeni.
“Asubuhi niliongea mambo ambayo niliwakwaza watu wenye familia zao,
si wote niliowakusudia kuwa ni mafuksa, wapo wachache naomba kuifuta
kauli yangu,” alisema Mbunge wa Viti Maalum, Mariam Msabaha (Chadema),
alipogundua kosa alilofanya kuwatuhumu wabunge wote na vitendo hivyo
vichafu.
Baada ya kufuta kauli huku akisisitiza bado baadhi ya wabunge wana
tabia hiyo, Mbunge wa Viti Maalum, Anna Abdallah (CCM), alimpongeza
Msabaha kwa kitendo chake cha kiungwana na kuamua kuomba radhi na kufuta
kauli yake kwani tayari ilishahatarisha ndoa za wabunge wengi ndani ya
Bunge hilo.
“Nampongeza Msabaha huu ndio uungwana naomba jambo hili liishe
umewaokoa akinababa wengi na akinamama ambao leo (jana) kutwa wameshinda
wakipigiwa simu na wenza wao wakiwahoji wewe wa kwako ni nani,”
alisema.
Kabla ya kauli hiyo, Mbunge wa Arumeru Mashariki Joshua Nassari
(Chadema), alitaka wabunge waache kuzungumzia masuala binafsi ya wabunge
ndani ya Bunge hilo, kwa kuwa endapo wabunge wote wakiamua kuzungumzia
masuala binafsi ya wabunge hao, Bunge hilo halitokalika.
“Kuna mambo mengi yanafanyika huko nje tukiyaleta humu ndani
hapatakalika, wapo watu wanahusishwa mambo chungu nzima ya uvunjifu wa
maadili, wapo hapa wanahusishwa kuwa wana uhusiano na watoto wadogo,
uongo, Bunge tunaliacha kama sehemu ya mipasho tuache haya jamani,”
alisema.
“Mimi ni mtoto mdogo, lakini nasema Bunge ni sehemu ya kujadili
masuala si sehemu kujadili watu au maisha ya mtu binafsi, anakula nini
au anafanya, ni sehemu ya kujali maslahi ya watu,” alisisitiza.
Details
Imechapishwa Ijumaa, 20 Desemba 2013 01:00
Imeandikwa na Mwandishi Wetu, Dodoma
No comments:
Post a Comment