Dar
es Salaam. Siku chache baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za
Serikali (PAC), Zitto Kabwe kutaja hadharani mishahara ya Rais Kikwete
na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, serikali imekataa kuizungumzia mishahara
hiyo.
Msimamo
wa Serikali kutotaja mishahara ya viongozi wakuu unatofautiana na
utamaduni wa nchi nyingine kama Marekani, Afrika Kusini, Ufaransa na
Kenya ambazo mishahara ya wakuu wake huwekwa wazi kwa umma.
Zitto
ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema akiwa wilayani Igunga Mkoani
Tabora, alisema Rais Kikwete anapokea zaidi ya Sh30 milioni kwa mwezi
(sawa na Sh360 milioni kwa mwaka) ikiwa ni marupuru na mshahara kwa
mwezi bila kodi, huku Pinda akipokea Sh 26 milioni kwa mwezi.
“Kuutaja
mshahara wa mtu mwingine ni kinyume cha sheria na kosa, siyo utaratibu.
Kwani wewe upo tayari watu waujue mshahara wako?” alihoji.
Aliongeza
kuwa ingawa mishahara ya viongozi hao inatokana na kodi za wananchi,
sheria ndiyo inayozuia watu kuyataja malipo hayo hadharani na kwamba
hayupo tayari kuutaja mshahara wa rais au kiongozi mwingine labda mtu
huyo autaje yeye mwenyewe.
“Siwezi kutaja mshahara wa bosi wangu wala wa kwangu mwenyewe. Wewe unaujua mshahara wa Obama (Rais wa Marekani)?” alihoji tena.
Akizungumzia
mishahara ya marais wa nchi nyingine duniani kuwekwa wazi, Kombani
alisema kila nchi ina utaratibu wake na kwamba Tanzania haijafikia hatua
hiyo.
Alipotafutwa
kulizungumzia suala hilo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue
simu yake ya mkononi iliita bila kupokewa. Gazeti hili pia liliwasiliana
na Naibu Mtendaji Mkuu mwenye jukumu la kuanzisha na kuongoza Idara ya
Mageuzi ya Kilimo Ofisi ya Rais Ikulu, Peniel Lyimo ambaye alisema yeye
si mhusika. “Masuala yote yanayohusu utumishi yapo Wizara ya Utumishi,”
alisema Lyimo.
Akianika
mshahara wa Waziri Mkuu, Zitto alisema kwamba kiongozi huyo analipwa
Sh11.2 milioni kama mbunge, Sh8 milioni kama waziri na Sh7 milioni kwa
nafasi yake ya Waziri Mkuu, hivyo, kumfanya kupokea zaidi ya Sh300
milioni kwa mwaka.
Hata hivyo, Kombani alilionya gazeti hili kuandika taarifa za mishahara ya watu kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Bashiru Ally alisema Mwalimu
Nyerere aliwahi kutaja mshahara wake hadharani na kuhoji viongozi
wanaotaka mishahara yao isitajwe wanaficha nini.
“Hata wakificha mishahara yao bado wananchi wataona maisha wanayoishi kuwa si safi,” alisema.
Wanaharakati pia wahoji
Mwenyekiti
wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba alisema siyo kosa
kwa mtu yeyote kutangaza mshahara wa viongozi wa umma kwa kuwa wanalipwa
kutokana na kodi za wananchi.
Aliongeza
kuwa kuanzisa sasa atakuwa balozi wa kutangaza mishahara ya viongozi
hao, ili kila mwananchi aweze kufahamu kama ambavyo imekuwa ikifanyika
katika nchi nyingine duniani.
“Ninachojua
mimi ni kuwa dhana ya mshahara inataka kuwepo na siri baina ya mwajiri
na mwajiriwa, lakini si kwa viongozi wa umma ambao wanalipwa na kodi za
wananchi. Kuanzia sasa hivi nitakuwa balozi wa kutangaza mishahara ya
viongozi hao ili kila mtu ajue,” alisema Kibamba.
Katibu
Mkuu wa Tanzania Labor Party (TLP), Jeremiah Shelukindo alisema ni
vyema kila mtu akaheshimu sheria inayozuia kutaja mshahara wa mtu
mwingine kwa kuwa kitendo hicho kinaweza kuwaudhi baadhi ya viongozi wa
umma.
“Si
vizuri kuingiza siasa kwenye mambo ya mishahara. Siyo mara ya kwanza
kusikia watu wakijaribu kutaja mishahara ya watu wengine huko ni kukiuka
sheria,” alisema.
Naye
Mkurugenzi wa asasi ya Sikika, Irenei Kiria alisema umefika wakati
ambapo inabidi uanze kufanyika mchakato wa kuzibadili sheria zinazolenga
kulinda masilahi ya viongozi wa umma.
“Tunataka kujua viongozi wanalipwa shilingi ngapi na kwa nini wanalipwa kiasi hicho,” alisema Kiria.
Nchi nyingine
Nchini Marekani, mshahara wa rais unajulikana tangu mwaka 1789 kiongozi wa nchi hiyo alipokuwa analipwa Dola 25,000 kwa mwaka.
Kuanzia 2001 hadi sasa, Rais wa Marekani analipwa Dola 400,000 (Sh 640 milioni) kwa mwaka, sawa na Sh 53.3 milioni kwa mwezi.
Rais
wa Afrika Kusini, Jacob Zuma analipwa Randi 2 ,917 038 sawa na zaidi ya
Sh400 milioni za Kitanzania kwa mwaka, Rais wa Ufaransa, Francois
Hollande Sh475 milioni, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron Sh338
milioni, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya Sh277 milioni na Rais wa Namibia,
Hifikepunye Pohamba Sh226 milioni kwa mwaka.
Wengine
na malipo wanayopata kwa mwaka ni Marais wa Urusi, Vladimir Putin,
Sh174 milioni, Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia Sh137 milioni, Michael
Satta wa Zambia, Sh126 milioni, Rais wa Angola, Jose dos Santos Sh91
milioni, Rais wa Lesotho, Profesa Pakalitha Mosisili Sh88 milioni,
Armando Guebuza wa Msumbiji, Sh84 milioni na Rais wa Jamhuri ya Watu wa
China, Xi Jinping Sh60 milioni.
Wengine
ni Rais wa India, Pranab Mukherjee Sh49 milioni, Rais wa Zimbabwe,
Robert Mugabe Sh27 milioni, Naibu Rais wa Afrika Kusini, Kgalema
Mothlanthe Sh331 milioni, Waziri Mkuu wa Namibia, Nahas Angula Sh160
milioni, huku Baba Mtakatifu wa Kanisa la Romani Catholic, Papa Benedict
XVI akifanya kazi bila kulipwa mshahara.
No comments:
Post a Comment