Rais Paul Kagame wa
Rwanda ameonya wale wote wanaokula njama za kuhatarisha serikali yake na taifa
kwa ujumla yatawageuka wenyewe kabla ya kufikia azma yao. Kauli ya Rais Paul
Kagame imekuja huku kukiendelea shutuma kutoka kwa wapinzani kwamba serikali
yake ikawa ilihusika na mauaji ya mkuu wa zamani wa ujasusi nchini Rwanda
Kanali Patrick Karegeya aliyeuwawa nchini Afrika Kusini. Serikali ya
Rwanda ilikanusha madai hayo.
Rais Kagame alitoa kauli
hiyo mjini Kigali kwenye kongamano la viongozi wa serikali na madhehebu
mbalimbali katika maombi ya kuliombea taifa na kumshukuru Mungu kwa mwaka
uliopita. Rais Kagame ambaye alikuwa mzungumzaji wa mwisho kwenye kongamano
hilo la siku moja amesema kamwe hatakuwa salama mtu yeyote atakayethubutu kuisaliti
Rwanda kwa lengo la kuangamiza maisha ya wanyarwanda wasio na hatia kwa maslahi
binafsi.
Amesema nchi hiyo
imetoka kwenye dimbwi la mauaji na mateso ya kila aina na kujijenga kufikia
hatua ilikofikia leo, huku akiongeza yeyote mwenye dhamira ya kubomoa mafanikio
hayo yatamgeuka mwenyewe kabla ya kufikia azma yake.
Alisema “Huwezi kulisaliti taifa
na ukadhani utakaa salama,yeyote atakayejaribu atakabiliwa na nguvu tulizopewa
na Mungu kuilinda nchi yetu.Yeyote atakayejaribu atakiona hata wale ambao bado
wako hai wasubiri - ni suala tu la muda”.
Bila kutaja majina Rais
Kagame amesema viongozi wa Rwanda wamekuwa wakitumia muda wao kukanusha shutuma
dhidi ya Rwanda kuhusu kifo cha mtu fulani akasema hata kama Rwanda haijahusika
lakini kwa nini watu hao waachwe ili waendelee na hujuma zao dhidi ya wananchi
wasio na hatia? Na wengi ni wale aliowataja kama waliosahau kilicho watoa
utumwani na sasa wanaigeukia nchi yao.
Kagame aliongeza na
kusema "wale wanaosahau kilichowatoa utumwani, ni lazima wakabiliwe na
athari ikiwa ni pamoja na hao mnaowasema, wamesahau wameshiba na kuvimbiwa
kisha kusahau kilichowapa umaarufu huo, lakini kumbe wakasahau kwamba nchi yao
Rwanda na Mungu aliyewaumba viko juu zaidi yao."
·
Rais Kagame ametoa tamko
hili huku kukiendelea wimbi la lawama kupitia vyombo vya habari kwamba serikali
ilikuwa na mkono kwenye mauaji ya mkuu wa zamani wa ujasusi nchini Rwanda
Kanali Patrick Karegeya. Rais na serikali ya Rwanda imekuwa ikikanusha vikali
kuhusika na mauaji hayo. Hata hivyo katika kuonyesha ukali wa shutuma
zake dhidi ya wapinzani alitoa mfano.
Akisema "watu wanaokuja hapa na
kurusha mabomu na kuua watoto wadogo wasio na hatia, polisi walioko wanafahamu
vipande vya miili ya watu wanavyookota baada kuuawa na mabomu kisha uniambie
niombe radhi?kamwe ."
No comments:
Post a Comment