Kitengo
cha Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini, kimewataja Agnes Gerald,
maarufu Masogange, na Melissa Edward kuwa watafuatiliwa nyendo zao kwa
umakini.
Hatua hiyo iliyotangazwa na Kamishna Mkuu wa kitengo
hicho, Geofrey Nzowa, imekuja siku moja baada ya Watanzania hao,
Masogange na Melissa kuachiwa huru na Mahakama ya Kempton Park ya Afrika
Kusini.
Nzowa alizungumza jana na mwandishi wa habari hii kwa
njia ya simu, kuwa watu hao wataangaliwa kwa umakini watakapokuwa
wakisafiri nje ya nchi.
Vilevile, alisema wataimarisha ukaguzi
kwa Watanzania wengine, wenye historia ya kubeba dawa za kulevya
wanaposafiri kwenda nje ya nchi.
“Masogange na Melissa
tutawaangalia kwa jicho la umakini zaidi watu hawa,lakini siyo hao tu
hata Watanzania wengine kwa sababu umdhaniaye siye kumbe ndiye,” alisema
Nzowa.
Nzowa alisema
Watanzania watakaokamatwa na dawa za kulevya nchini au nje na
wataadhibiwa kulingana na sheria kama Masogange alivyoadhibiwa.
Hata
hivyo, juzi Nzowa alionyesha kushangazwa na hukumu waliyopewa Masogange
na Melissa akisema kuwa ni ndogo ukilinganisha na kiasi kikubwa cha
kemikali walizobeba.
Hapa jijini Johannesburg, Masogange na
Melissa jana walionekana wakitembelea maeneo mbalimbali ya jiji hilo
ikiwamo madukani wakifanya ununuzi na katika saluni za urembo.
Mtu
wa karibu na watu hao alisema, Watanzania hao hawana hofu ya kufanya
chochote kwa sababu mahakama imegundua kuwa hawana hatia.
“Waogope
kutembea barabarani kwa sababu gani wakati wameachiwa huru? Mahakama
imefanya kazi yake na wao wana haki,” alisema mtu huyo ambaye hakutaka
jina lake liandikwe gazetini.
Julai 5 mwaka huu, Masogange na
Melissa walikamatwa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Oliver Tambo Afrika
Kusini wakiwa wamebeba kilo 150 za dawa za kulevya aina ya crystal
methamphetamine (Tik).
Hata hivyo, baada ya kukaa mahubusu kwa
takriban miezi mitatu, mahakama ya Kempton inayoshughulikia makosa ya
jinai, ilibaini kuwa Watanzania hao hawakubeba dawa za kulevya bali
kemikali zinazotumika kutengeneza dawa za kulevya aina ya ephedrine.
No comments:
Post a Comment