Mbunge wa Chadema Zitto Kabwe
KUBORONGA kwa Simba Ligi Kuu Bara kumekoroga mambo ndani ya klabu hiyo.
Mwenyekiti
wa Simba, Ismail Aden Rage amevunja kamati zilizokuwa zinaundwa na
waziri na wabunge kadhaa. Rage pia amelifuta tawi maarufu la Mpira Pesa
la Magomeni jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam jana Ijumaa kwenye Makao Makuu ya Simba,
Rage alidai amechukua hatua hiyo ili kurudisha utulivu klabuni na
kuongeza ufanisi.
Fagio hilo limewakumba Naibu Waziri wa
Habari, Utamaduni na Michezo, Amosi Makala, Mbunge wa Kigoma Kaskazini
(Chadema), Zitto Kabwe, Mbunge wa Kilwa-Kusini (CCM), Murtaza Mangungu
na Mbunge wa Kilombero (CCM), Abdul Mtekete, aliyewahi kuichezea Simba
na Pan African.
Vigogo hao walikuwa wajumbe wa Kamati ya Fedha na Uchumi iliyokuwa chini ya Makamu Mwenyekiti, Geofrey Nyange 'Kaburu'.
Kamati
nyingine zilizovunjwa ni ya usajili, ambayo bosi wake alikuwa Zacharia
Hans Pope, Kamati ya Mashindano chini ya Joseph Kitang'are 'Mzee
Kinesi', Ufundi iliyokuwa inaongozwa na Ibrahim Masoud 'Maestro' na ya
Nidhamu iliyokuwa chini ya Peter Swai.
Rage alisema wanachama
wa Mpira Pesa, wamekuwa wakihusika kupitisha karatasi la saini za
wanachama ili kuitisha mkutano bila idhini ya Kamati ya Utendaji kinyume
cha katiba ya Simba.
Alikwenda mbali zaidi na kutangaza
kuwang'oa Mwenyekiti wa tawi hilo, Masoud Awadhi na anayejiita
Mwenyekiti wa Wanachama, Ally Bani kwa kukiuka katiba ya Simba.
Wanachama
hao walishiriki kutembeza karatasi lililofikisha saini zaidi ya 700 na
walikuwa na uwezo wa kuitisha mkutano wa wanachama ili kuupindua
uongozi.
Rage alisema katika uchunguzi wao pia wamegundua watu
zaidi ya 80, si wanachama hai na wengi walikuwa wanatumia stakabadhi
feki kulipia ada ya uanachama.
"Tumewaruhusu kuunda tawi jingine kama watajikusanya tena," alisema Rage.
Hata
hivyo, Awadh alijibu mapigo kwa kudai kuwa wao walifuata katiba kwa
kuomba saini za wanachama waliofika 700 kama katiba inavyotaka na
ameahidi kupeleka suala lao kwa Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo wa
Wilaya ya Ilala.
No comments:
Post a Comment