Ndugu Wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Napenda
nichukue fursa hii kuwajulisha rasmi kwamba Nchi yetu imepata heshima
ya kutembelewa na Waziri Mkuu wa Thailand ambaye atawasili Nchini tarehe
30/07/2013. Ziara hii ni ya kikazi (state visit) na atawasili katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kumbukumbu ya Mwalimu J. K. Nyerere
majira ya saa 6:30 mchana na kulakiwa na mwenyeji wake Mhe. Rais wetu
mpendwa Dr. Jakaya Mrisho Kikwete akifuatana na Viongozi mbalimbali wa
Kitaifa na Mkoa.
Ndugu Wananchi,
Baada
ya kuwasili Mhe. Waziri Mkuu wa Thailand atakagua gwaride maalum
lililoandaliwa kwa ajili yake na pia atapata fursa ya kukagua vikundi
mbalimbali vya ngoma ambavyo vitakuwa vikitumbuiza na kutoa burudani kwa
Mgeni wetu na msafara wake.
Ndugu Wananchi,
Mgeni
wetu baada ya kukagua vikundi vya ngoma na burudani ataondoka kuelekea
Ikulu kupitia barabara ya Nyerere, Railway, Gerezani, Sokoine Drive hadi
Ikulu. Akiwa Ikulu atasaini mikataba mbalimbali kati ya Serikali ya
Tanzania na Thailand. Usiku atashiriki katika dhifa maalumu
iliyoandaliwa na Mwenyeji wake.
Endelea kusoma habri hii kwa kubofya hapa chini
Ndugu Wananchi,
Tunaomba
radhi kwamba barabara hizi nilizozitaja zitafungwa kwa muda kupisha
misafara ya Viongozi wetu Wakuu watakaoelekea Uwanja wa Ndege wa
Kumbukumbu ya Mwalimu J. K. Nyerere kumlaki Mgeni wetu hususan barabara
ya Nyerere kuanzia saa 6.00 mchana hadi saa 7.30 mchana.
Ndugu Wananchi,
Tarehe
31/07/2013 Waziri Mkuu wa Thailand atatembelea Mbuga za Wanyama za
Serengeti.Tarehe 01/08/2013 atarejea Dar es Salaam na kuagwa rasmi
katika Uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere na kuendelea na ziara yake huko
Uganda.
Ndugu Wananchi,
Kama ilivyo ada tunaombwa kumlaki mgeni wetu kwa shangwe na bashasha katika maeneo yote atakayopita.
Asanteni kwa kunisikiliza.
Saidi Meck Sadiki
MKUU WA MKOA
DAR ES SALAAM
No comments:
Post a Comment