Na Ibrahim Yamola, Mwananchi
CCM imewatia hatiani vigogo wote sita kwa makosa
ya kujihusisha na kampeni za uchaguzi kabla ya wakati, hivyo kuwafungia
kugombea nafasi za uongozi ndani ya chama hicho kwa miezi 12, pia wakiwa
chini ya uangalizi.
Waliokumbwa na adhabu hiyo ni Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano
na Uratibu), Stephen Wassira, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na
Madini, William Ngeleja.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
akizungumza na waandishi wa habari jana alisema wanachama hao wote sita
walitiwa hatiani kwa makosa ya kuanza kampeni za kuusaka urais wa 2015
kabla ya wakati jambo ambalo ni kinyume na taratibu za chama hicho,
hivyo kutoa onyo kali. Adhabu ya onyo kali kwa mujibu wa taratibu za
chama hicho inamaanisha kuwaweka chini ya uangalizi kwa miezi 12 ili
kuhakikisha hawajihusishi na vitendo vyovyote vinavyokwenda kinyume na
misingi ya chama hicho, vinginevyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
“Mwanachama aliyepewa onyo kali atakuwa katika
hali ya kuchunguzwa kwa muda usiopungua miezi 12 ili kumsaidia katika
jitihada zake za kujirekebisha,” alisema Nnauye.
Hatua hiyo ya CCM imezitia doa harakati za vigogo
hao, kwani watatumikia adhabu yao hadi Februari 2015 na wakati wote
watakuwa wakichunguzwa mienendo yao.
Nnauye alisema makada hao kwa kuanza kwao kampeni
za kutafuta kuteuliwa kuwania urais kabla ya wakati ni kinyume na kanuni
za uongozi na maadili za CCM, toleo la Februari 2010, Ibara 6 (7)(i).
“Wamethibitika kufanya vitendo vinavyokiuka
maadili ndani ya chama na baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka
maadili ndani ya jamii. “Vitendo vya namna hii ni kosa kwa mujibu wa
kanuni za uongozi na maadili za CCM toleo la Februari 2010, Ibara kadhaa
za kanuni hizo,” alisema Nnauye.
Alisema: “Kamati Kuu baada ya kuthibitisha makosa
hayo, imewapa watu wote sita waliohojiwa adhabu ya onyo kali na kuwataka
wajiepushe na vitendo vinavyokiuka maadili na iwapo wataendelea na
vitendo hivyo chama kitawachukulia hatua kali.”
Alisema Kamati Kuu imeiagiza kamati ya maadili
kuwachunguza mawakala na watendaji wa wanachama hao waliokuwa wakiratibu
shughuli mbalimbali ili waweze kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu
hatua inayolenga kuhakikisha chama hakigawanyiki.
Nnauye alisema Ibara 6 (2) (1-5) ya maadili ya
viongozi wa chama hicho inawazuia kutoa michango, misaada, zawadi za
aina yoyote, kukusanya michango na kufanya kampeni bila ya kupata kibali
kutoka kamati ya siasa ya halmashauri ya eneo husika.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment