Pages

Ads 468x60px

LIKE THIS PAGE FIRST.

Tuesday, March 11, 2014

HUJAFA HUJAUMBIKA.....OMBI LA MSAADA KWA MZEE HUYU MWENYE TATIZO HILI

Ngaweje Said anayeteseka na gonjwa asilolijua.

WANASEMA ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni, ni kweli! Ngaweje Said (39), mkazi wa Kijiji cha Zinga, Bagamoyo, Pwani anateseka na gonjwa asilolijua ambapo nyama kubwa imeota toka juu ya uso upande wa kushoto na kumwagikia kifuani, Uwazi lilikutana naye uso kwa uso. Akizungumza na mwandishi wetu akiwa nyumbani kwake kijijini hapo juzi, Ngaweje alisema:“Ugonjwa huu ulinianza nilipozaliwa tu mwaka 1975 pale Hospitali ya Bagamoyo. Kilianza kipele, lakini kadiri nilivyokuwa nikikua, kipele nacho kilikua.

“Sikujua kama itafikia hali hii. Hata wazazi wangu nao hawakujua, waliamini baada ya tiba kipele kitanywea, lakini wapi!
“Baadhi ya watu walishauri nipelekwe Hospitali ya Muhimbili ambako kuna madaktari bingwa. Kweli, mwaka 1979, baba alinipeleka Muhimbili ambako nilipata tiba na kurudi nyumbani lakini kipele kilizidi kukua.
“Mwaka 1995, mimi mwenyewe nilirudi tena Muhimbili. Safari hii madaktari waliniambia watanifanyia upasuaji kwa awamu.
“Walinifanyia upasuaji, wakaniruhusu kurudi nyumbani ili nikatafute fedha halafu nirudi tena lakini hawakuniambia ni shilingi ngapi na pia sikupata hiyo pesa!
“Mwaka 2001 sasa ikiwa si kipele tena bali ni linyama likubwa, niliamua kwenda Hospitali ya CCBRT, (Msasani, Dar). Pale pia wakaniambia nikatafute pesa halafu nirudi wanifanyie upasuaji.
“Sikuwa na fedha kwa sababu sikuwa na kazi yoyote ya maana, ni kama nilivyo sasa. Kuanzia hapo niliamua kuachana na hospitali nikimtegemea Mungu atakavyoamua.
“Mbaya zaidi wazazi wangu walishafariki dunia. Alianza baba, akaja mama kwa hiyo nikawa sina msaada wowote ule.
“Nilipanga kuoa nikiamini kwamba mke atanisaidia, lakini wanawake wananikataa kwa hali yangu. Na ukiangalia ni kweli, mke gani atakuwa tayari kuishi na mume mwenye linyama kama hili, tena usoni?
“Kwa sasa nahangaika tu, nafanya biashara ya kuchajisha simu za watu kwa shilingi 200 kwenye chumba nilichopewa. Kwa siku wanaweza kuja wateja wanne ambapo napata shilingi 800 tu, hainisadii chochote.
“Kusema ukweli jamani mimi nakufa, lakini kama Watanzania wenzangu mpo na mtaguswa na gonjwa langu hili naombeni mniokoe. Kuna watu wanasema nikienda India wanaweza kunifanyia upasuaji nikawa kama binadamu wengine, lakini nitaendaje huko wakati sina fedha?”
Simulizi ya Ngaweje inaumiza sana, hata mazingira anayoishi si ya kuridhisha. Anasema anahisi kichwani ana mzigo mzito kutokana na nyama hiyo kumwelemea.
Anasema: “Hata nikitembea nahisi kuzidiwa upande mmoja. Nafsi yangu imekuwa ikijitenga na watu kwa sababu naamini siko kamili na pia nahisi nawakera wanaponiona.”
Ngaweje anahitaji shilingi 5,000,000 ili kufanyiwa upasuaji nje ya nchi. Kwa wale watakaokuwa tayari kumsaidia kwa njia moja au nyingine, wanaweza kuwasiliana naye kwa namba yake ya simu ya mkononi (Tigopesa) 0659764461.
Kuwasaidia wenye shida ni sehemu ya Ibada kwa imani zote za dini, ndugu yangu jichotee baraka kwa kumsadia ndugu yetu huyu ambaye kiukweli yupo kwenye mateso mazito.

No comments:

Post a Comment