Miraji
Kikwete na Aima Mahmoud wakiondoka kwenye ukumbi wa Mlimani City baada
ya kufunga ndoa yao jana. Picha na Florence Majani
Shamra
shamra na nderemo zilitawala jana kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani
City wakati Miraji Kikwete, mtoto wa Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete
alipofunga ndoa na Alma Mahmoud.
Sherehe hizo zilianza saa 7:00 mchana baada ya ndoa kufungwa na maharusi hao kuingia ukumbini hapo wakiongozana na Rais Kikwete.
Hali
nje ya ukumbi huo ilikuwa tulivu ingawa uwanja ulikuwa umefurika magari
ya polisi, viongozi na wageni waalikwa. Huku kikosi cha kudhibiti
ulinzi na usalama kikiwa kimefunga mitambo ndani na nje ya ukumbi huo.
Ulinzi
katika eneo hilo ulikuwa ni mkali kupita kiasi ambapo hakuna yeyote
aliyeruhusiwa kuingia ukumbini humo bila kadi maalumu, hata angeomba kwa
kupiga magoti.
“Hata
sisi tumetoka Bagamoyo hadi hapa tuna undugu kabisa na mkubwa (Rais
Kikwete), lakini wametunyima kwa sababu hatuna kadi,” alilalamika
mwanamke mmoja aliyeongozana na wanaume wawili.
Hakuna
waandishi wa habari walioruhusiwa kuingia ndani ya ukumbi huo,
isipokuwa waandishi na wapiga picha maalumu wa Serikali ambao walipewa
vitambulisho maalumu na tisheti.
Wengine
walioonekana wakipiga picha ni wanafamilia ambapo watoto wa kiume wa
Rais Kikwete, walionekana wakiwa na kamera huku wamevalia kanzu nadhifu.
Mfanyakazi
mmoja wa Ikulu alipomwona Mwandishi wa gazeti hili, alimfuata na
kumwambia kuwa sherehe hiyo ni ya kibinafsi na haruhusiwi mwandishi
yeyote kufanya kitu chochote.
“Tumenyimwa
kuruhusu waandishi kwenye sherehe hii, sawa wewe ni mwandishi lakini
hii ni sherehe binafsi na ya kifamilia, huruhusiwi kupiga picha yeyote,”
alisema mfanyakazi huyo, jina linahifadhiwa.
Hata
hivyo, mwandishi alitumia mbinu kupata picha za maharusi hao pamoja na
matukio mengine yaliyokuwa yakiendelea ukumbini hapo.
Wageni wengi waalikwa walianza kuingia ukumbini humo majira ya mchana na wengine waliendelea kuwasili hadi saa 11 za jioni.
Miongoni
mwa viongozi wa kitaifa waliohudhuria sherehe hizo ni pamoja na Makamu
wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi,
Waziri wa Afya, Dk Hussein Mwinyi, Naibu Waziri wa Afya, Dk Seif Rashid
na Waziri wa Maendeleo ya Wanawake Jinsia na Watoto, Sophia Simba.
Wengine
waliokuwepo ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu, Inspekta Jenerali Omari
Mahita, Mkurugenzi wa Mashindano ya Urembo ya Miss Tanzania, Hashim
Lundenga, Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Issa Shaaban Simba na Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadicky.
Muda
wa chakula ulianza mida ya saa kumi jioni ambapo baada ya bwana na bibi
harusi kuchukua chakula, wageni waalikwa nao walianza kuitwa kwa
makundi na kwa ustaarabu wa hali ya juu kuchukua chakula.
Hata
hivyo kutokana na wingi wa watu waliofurika ukumbini hapo, msururu wa
chakula haukumalizika hadi Miraji na mke wake mpya wanaondoka ukumbini
hapo.
Rais
Kikwete ambaye alikuwepo katika sherehe hiyo alikuwa wa kwanza kuondoka
ukumbini hapo muda wa saa 11:30 jioni akifuatiwa na Rais Mwinyi na
viongozi wengine wa kitaifa.
Maharusi
walikuwa wa mwisho kutoka ukumbini baada ya viongozi wote wa kitaifa
kuondoka huku wimbo maarufu wa “Aiya iyaaa kuolewa utarudi nyumbani
kutembea” ukiwasindikiza jambo ambalo bila shaka lilimuumiza bibi harusi
huyo ambaye alianza kulia huku Miraji akionekana kumbembeleza.
Baada ya Alma kuingia kwenye gari, Miraji naye aliingia akiwa anacheza kwa furaha huku Ridhwani akimfungulia mlango.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment