Profesa Faustine Lekule
CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimehadharisha walaji wa
nyama ya nguruwe nchini, kuwa wanakabiliwa na hatari ya kupata kifafa.
Utafiti wa kisayansi uliofanywa na SUA, umebaini kuwa baadhi ya
nguruwe wana minyoo aina ya tegu ambao nyama yao ikiliwa bila kuiva
vizuri, mlaji atapata minyoo hiyo ambayo huingia kichwani na kusababisha
kifafa.
Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, Mhadhiri na Mtafiti wa
Idara ya Sayansi ya Wanyama na Uzalishaji ya SUA, Profesa Faustine
Lekule, alisema sampuli za utafiti huo kutoka Mbeya, zimebaini nguruwe
wengi wakiwamo wanaosafirishwa katika miji mikubwa wameathirika na
minyoo hiyo.
Kwa mujibu wa Profesa Lekule, wataalamu wa SUA wanaosimamia Mradi wa
Utafiti wa Kuboresha Ufugaji wa nguruwe kwa mkoa wa Mbeya ili kuinua
pato la kaya, unaofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la
Denmark (DANIDA), walibaini hatari hiyo baada ya kuchukua sampuli ya
nyama ya nguruwe kwa ajili ya vipimo.
“Majibu ya sampuli ambazo wataalamu wamezichukua kutoka kwa nguruwe
wa wafugaji kwenye baadhi ya vijiji, wamebainika kukumbwa na hatari hii.
“Lazima jitihada za makusudi zichukuliwe katika kutafuta ufumbuzi wa
pamoja wa tatizo hili kati ya watafiti na Serikali,” alisema Profesa
Lekule.
Alisema maambukizi ya tegu au minyoo ya nguruwe yanatokana na tabia
za baadhi ya wafugaji kutozingatia ufugaji bora kwa kuwaacha kujitafutia
chakula na maji mitaani na kula kinyesi cha binadamu.
Kwa mujibu wa Profesa Lekule, baadhi ya wafugaji wamekuwa
wakijisaidia vichakani na kuwaacha nguruwe kutafuta malisho katika
vichaka na kula kinyesi chao, hali inayochangia ongezeko la maambukizi
ya minyoo ya tegu hao.
Baada ya kula kinyesi minyoo humwingia mwilini na kumdhoofisha na
baadaye binadamu anapokula nyama ambayo haijaiva vizuri, minyoo hiyo
humwingia na kusababisha kifafa baada ya kuingia kichwani.
Alisema athari za kuenea kwa maambuziki hayo inaweza kutokea katika
miji mikubwa ikiwamo Dar es Salaam kwa kuwa nguruwe wa Mbeya
husafirishwa na kuuzwa maeneo hayo.
“Hatua hii inaweza kusababisha kusambaa kwa ugonjwa huu, hivyo
ushirikiano kati ya wafugaji, wafanyabiashara, Serikali na wataalamu wa
afya katika kufikia hatua ya kumaliza changamoto hii unahitajika,”
alibainisha Profesa Lekule.
No comments:
Post a Comment