Pages

Ads 468x60px

LIKE THIS PAGE FIRST.

Tuesday, November 26, 2013

MNIGERIA MBARONI NA KILO NNE ZA DAWA ZA KULEVYA......!!


Wiki  moja tangu Waziri wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe atishie kuwafukuza kazi maofisa wa idara za usalama watakaobainika kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya kupitishwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Polisi imemnasa raia wa Nigeria, Chubuzo John, akiwa amebeba dawa hizo zenye uzito wa kilogramu nne.

Chubuzo aliyekuwa akisafirisha dawa hizo kupitia uwanja huo, alikamatwa muda mfupi kabla ya kutaka kuondoka na ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia kuelekea Roma, nchini Italia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alithibitisha kukamatwa kwa Chubuzo kwa tuhuma hizo.

Alisema raia huyo wa Nigeria alikamatwa wakati wa ukaguzi wa mizigo akiwa amefungasha dawa hizo kwenye mikoba yake tayari kuzipeleka nchini humo.

“Bado hadi sasa hatujafahamu ni aina gani ya dawa za kulevya alizokuwa akizisafirisha kwenda Roma (Italia). Na hivi sasa tunamshikilia kwa mahojiano. Huyu Mnigeria alikamatwa na polisi juzi saa 11:45 jioni akijiandaa kuvusha dawa hizo alizokuwa amezipaki katika mizigo yake,” alisema Kamanda Boaz.

Hadi jana mchana, polisi walikuwa wamezipeleka dawa hizo kwa Kamishna wa Dawa za Kulevya nchini, ili kubaini ni aina gani ya dawa za kulevya zilizokuwa zikisafirishwa kupitia uwanja huo uliopo Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.

“Hizo dawa tumempelekea Kamishna wa Dawa na yeye ndiye atakayesema thamani yake ni kiasi gani na ni aina gani ya dawa alizokamatwa nazo huyu raia wa Nigeria kabla ya kumburuza kortini kusomewa mashitaka yanayomkabili kwa mujibu wa sheria za nchi,” alisema Kamanda Boaz.

Wiki iliyopita, Dk. Mwakyembe alifanya ziara ya kushtukiza KIA na kuwaonya maofisa wa idara za usalama pamoja na maofisa wa umma kutougeuza uwanja huo kuwa uchochoro wa kupitisha dawa za kulevya.

Pia aliwaonya maofisa wa idara ya uhamiaji kutojihusisha na biashara hiyo haramu kwa kuwa siku zao zinahesabika.

Dk. Mwakyembe alisema anatambua wafanyabiashara wa dawa za kulevya wanaitumia KIA kama njia ya kusafirisha kwenda ughaibuni na kuwataka wanaoendesha biashara hiyo haramu kuacha kwa kuwa serikali itachukua hatua kali dhidi yao.

Alisema taarifa zinaonyesha kuwa Watanzania wengi na wageni wanaokamatwa ughaibuni wakiwa na pasi feki za kusafiria, nyingi huonyesha zimetokea KIA.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment