SAKATA la mabilioni yanayodaiwa kufichwa na Watanzania nje ya nchi jana
lilileta zogo bungeni baada ya Mwanasheria Mkuu, Jaji Frederick Werema,
kutifuana na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, huku Mbunge wa
Arusha Godbless akiwataka wote wawili wampe majina ayataje hadharani
kama wanashikwa na woga.
Huku Zitto akisisitiza kuwa serikali haionyeshi nia ya kuwachukulia
hatua walioficha pesa hizo nje ya nchi, Jaji Werema aliliambia Bunge
kuwa Zitto mwenyewe ameshakiri chini ya kiapo ofisini kwake kwamba hana
majina wala akaunti za watu hao, kinyume cha kauli yake huko nyuma
alipowahi kusema kuwa anawajua.
Kwa mujibu wa Jaji Werema, kwa kuwa sakata hili liliibuliwa bungeni na
Zitto, serikali iliunda kamati malumu ikitarajia kuwa mbunge huyo ndiye
angetoa ushirikiano kurahisisha uchunguzi huo, lakini mara zote amekuwa
akiikwepa kamati.
Alisema Zitto anapotosha Bunge na taifa kuhusu sakata hilo. Kauli ya
Werema ilitolewa jioni wakati Bunge limekaa kama kamati, akijibu hoja ya
Zitto aliyoitoa asubuhi akiishutumu serikali kwa kutokuwa na nia
thabiti ya kufuatilia pesa hizo ili zirejeshwe.
Lakini kabla ya Mwanasheria Mkuu kujibu, Lema alikuwa amewataka serikali
na Zitto kuacha kuchezea akili za Watanzania; kwamba wawe na ujasiri wa
kutaja wahusika badala ya kupiga danadana.
Lema alisema kuwa kama wao wanaogopa kutaja wahusika, basi apewe yeye
majina awataje hadharani, kwa maana hahitaji kinga ya Bunge kutaja wezi
wa mali ya umma.
Jaji Werema alisisitiza kuwa Zitto ameshakiri chini ya kiapo ofisini kwa
Mwanasheria Mkuu, kuwa hana majina wala akaunti yoyote iliyoko Uswisi.
Katika kusisitiza hoja yake, Jaji Werema alitoa mlolongo wa vikao
ambavyo kamati iliyoundwa na serikali kuchunguza sakata hilo ulivyokuwa
ukifanya, lakini Zitto alikuwa akiipiga chenga kabla ya kukiri kuwa hana
majina wala akaunti.
“Kauli alizozitoa Mheshimiwa Mbunge Zitto Kabwe, kwamba serikali haina
nia ya kurejesha fedha zilizofichwa nje, haziendani na tabia yake,
haziendani na mwenendo wake na haziendani na kauli zake mbele ya kamati
kwa sababu tumemuita mara kadhaa mbele ya kamati lakini hatokei.
Alisema kamati ilipoundwa, ilikuwa na majukumu ya kuchunguza kama fedha
hizo ni haramu, kutambua benki zilikofichwa fedha hizo, kutambua
waliozificha, kuandaa mashtaka na kisha kuishauri serikali.
“Februari 28, mwaka huu, kamati ilikutana hapa bungeni katika ofisi
yangu na ilipomuita Mheshimiwa Zitto aje atoe ushahidi, alikuja
akatwambia anazo nyaraka na taarifa ila akaomba ahakikishiwe usalama ili
pale ambapo angezileta pasingelikuwa na mtu wa kumzonga.
“Pia, alitaka mimi nitoe kiapo ambacho baada ya kutaja hayo majina
halafu ikawa siyo kweli, basi yeye awe ‘free’ (huru), kwa hiyo alitaka
apewe kinga ya kiapo.
“Machi 23 tulipomuita aje akatukwepa, akasema anakwenda Tanga kwenye
mafunzo ya mgambo, kwa hiyo, tukaona tumsubiri hadi atakapomaliza.
“Aprili 12, mwaka huu, tukakutana naye hapa Dodoma katika viwanja vya
Bunge, akasema hawezi kutwambia chochote kwa sababu alikuwa akijiandaa
kwenda Afrika Kusini.
“Mei 4 tulimuita tena kwenye kamati hapa Dodoma na katikati ya mahojiano
alidai ana jambo muhumu lenye maslahi kwa taifa, akasema anaomba
aondoke atarudi, kamati ilimruhusu, hata hivyo hakurudi tena.
“Tulipompigia simu alisema alikuwa Dar es Salaam na alikuwa ‘busy’ akijiandaa kwa kongamano la Kigoda cha Mwalimu Nyerere.
“Mei 24 kamati ilimfuata Dar es Salaam, akasema hana nafasi kwa sababu
wakati huo alikuwa akijiandaa kuisaidia Timu ya Taifa,” alisema Jaji
Werema na kuongeza:
“Kamati iliamua sheria ichukue mkondo wake kwa mujibu wa Sheria ya
Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Kifungu cha sita ndipo tukachukua maelezo
ya Zitto Kabwe chini ya kiapo na akatwambia hakuwa na jina, wala akaunti
ya Mtanzania yeyote aliyeficha fedha nje.
“Lakini, leo hapa amesema serikali haina nia ya kurudisha fedha
zilizofichwa Uswisi. Kwa maana hiyo, Mheshimiwa Naibu Spika, Zitto Kabwe
ni mzito na nakubaliana na Lema (Mbunge wa Arusha Mjini) aliyesema
hapa, kwamba Zitto alete majina hayo.
“Katika hili, nawashukuru wabunge 87 waliofika mbele ya kamati,
nawashukuru wananchi wengine waliofika kwani sasa tumefika pazuri ila
serikali inaomba iongezewe miezi sita ili ikamilishe jambo hili lakini
hili suala la Zitto tutashughulika nalo kisheria kwa sababu huwezi
kulidanganya Bunge halafu ukaachwa,” alisema Jaji Werema.
Kwa mujibu wa Werema, baada ya kamati kuona Zitto haipi ushirikiano,
iliamua kumuandikia barua rasmi kwa wito maalumu ofisini kwa Mwanasheria
Mkuu wa Serikali.
Werema alisema kuwa Zitto aliitikia wito huo, na akazungumza na kamati
chini ya kiapo, kwamba hana majina wala akaunti za Watanzania zilizo
Uswisi.
Kutokana na hali hiyo, Werema alisema hakuelewa ni kwa nini Zitto
alisema jana bungeni kwamba serikali inakataa kuchukua hatua, huku
akijua kuwa ndiye aliyeanzisha suala hilo, na amekuwa anakwepa vikao na
kamati iliyoundwa kumsaidia kuchunguza suala hilo, ambalo tayari
ameiambia kamati kuwa hana majina wala akaunti.
No comments:
Post a Comment